Dar es Salaam. Umeshawahi kujiuliza kwa nini Rais John Magufuli hanenepi? Wakati ukitafakari hilo, jana kiongozi huyo mkuu wa nchi ameweka wazi siri ya kutonenepa kwake.
Aliweka wazi siri hiyo katika ziara yake ya siku nane mkoani Mbeya, akisema madaraka aliyonayo yanamnyima usingizi kwa kujiona kuwa na deni kubwa kwa Watanzania, huku akitaja mambo matano aliyosema kuwa yanamfanya asinenepe.
Akizungumza katika Uwanja wa Mwakangale wilayani Kyela, kiongozi huyo alisema wananchi wanapaswa kutambua Serikali iliyopo madarakani hailali usiku na mchana, inafanya kazi kwa faida yao na waangalie walipotoka, walipo na wanakokwenda.
Alianza kwa kuelezea miradi mbalimbali ya maendeleo na namna Serikali ilivyoitekeleza, akisema ni wakati sasa Watanzania wafanye tathmini ya yale yaliyofanywa.
Mambo hayo ni miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege, afya, elimu na ajira.
“Unafanya hiki unamaliza unaingia kingine, haiwezekani ukavifanya vyote unatengeneza barabara yenye gharama ya Sh60 bilioni unamaliza, huku umeme unakusubiri kila mahali unaweka, elimu bure, huku unaajiri madaktari, walimu kule, unajenga vituo vya afya ndiyo maana nashindwa hata kunenepa,” alisema Rais Magufuli.
Alisema miradi ni mingi kwani mwanzoni mwa mwezi huu akiwa katika ziara yake mkoani Ruvuma alizindua vituo vya afya 352 vilivyoboreshwa vikiwamo 67 vipya.
“Vituo vya afya Tanzania nzima vimekamilika havikujengwa na hewa, ni fedha za walipakodi mkiwamo ninyi, fedha hazikutolewa na wafadhili wowote, tungewapelekea wasingetoa tumejenga kwa gharama zetu. Umeme kwa fedha za Watanzania kwa asilimia 100. Fedha hizo zimepatikana baada ya kuwabana mafisadi na wala rushwa.”
Rais alisema, “tumewabana mafisadi ndiyo maana tumepata tusingefanya hivyo tusingefanikiwa. Tumeamua kupambana na wala rushwa na hiyo ni kazi ngumu kwa kuwa hawana alama katika uso, unaweza kukuta mwana CCM kumbe ni fisadi, Chadema kumbe fisadi kwelikweli.”
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza fedha za kununulia dawa kutoka Sh31 bilioni mpaka Sh270 bilioni na elimu bure kila mwezi Sh23.86 bilioni.
“Tunafanya haya kuhakikisha kila mwenye haki anapata haki yake, tumenunua ndege nane kwa mpigo tena mpya watu walipiga vita mno, mara kwa nini hatukopi, unayo fedha cash (taslimu) unakopa ya nini?” alihoji. Rais Magufuli alisema kwa sasa kuna upanuzi wa viwanja 11 vya ndege.
“Tunataka maparachichi yabebwe moja kwa moja hadi kwenye masoko zitue, ndege kubwa za kwenda Ulaya hapa Kyela, unamkuta mtu mmoja amelewa tikiti maji anaongea vitu havieleweki.”
Alisema, “Tanzania ni nchi ya mfano kwa sasa, ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kiwango kikubwa mno, haya yote shetani hajalala wapo watakaotamka ambayo hata hayatakiwi, wapo watakaoona wivu kwa nini yanatokea.”
Katika ziara yake jana, Rais Magufuli aliagiza Sh3 bilioni zitengwe kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha ujenzi wa upanuzi wa kituo kikubwa cha Forodha na Uhamiaji Kasumulu na kumtaka katibu mkuu Wizara ya Ujenzi kuhakikisha anawalipa fidia wananchi wanaostahili kuanzia leo.
Baada ya kumaliza mkutano huo alikwenda katika Chuo cha Ualimu Mpuguso wilayani Rungwe na kupokewa kwa mabango ambayo aliwataka viongozi kumuacha ayasome.
Rais Magufuli aliagiza viongozi nchini kuhakikisha wanapanga utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi na kuwatembelea watu wanaowaongoza ili kutatua migogoro mbalimbali nchini.
0 comments:
Post a Comment