Ratiba ya uteuzi wa wa Spika wa Bunge la 11 pamoja na Waziri mkuu sasa iko hadharani.Ratiba hiyo inaonesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitalazimika kumtaja mgombea wake atakayekuwa na nafasi kubwa ya kuwa Spika kati ya kesho na keshokutwa huku wananchama waliojitokeza hadi sasa wakiwa 22.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kuanzia jana mpaka kesho, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watapaswa kuwa wameshawasili mjini Dodoma na kujisajili kwa watumishi wa Bunge ambao wameshaanza kazi hiyo.
Ratiba ya Bunge hilo imeonesha kuwa keshokutwa siku ya Jumatatu, wabunge wote wanatarajiwa wawe wameshajisajili ili saa nne asubuhi washiriki kikao cha maelekezo katika Ukumbi wa Bunge kitakachohusisha kutembelea ukumbi huo.Siku hiyo hiyo kuanzia saa 10 jioni, wabunge hao watakuwa na mikutano ya vyama vyao, ambako inatarajiwa hoja kubwa itakuwa jina la Spika na Naibu Spika.
Aidha,siku ya jumanne kikao cha Kwanza cha Bunge la 11 ambacho kitatanguliwa na kusomwa kwa tamko la Rais Magufuli la kuitisha Bunge kitaanza.
Mara baada ya kusomwa kwa tamko hilo, kutafuatiwa na uchaguzi wa Spika utakaofanyika kwa kura za siri na mshindi akishatangazwa, atakula kiapo siku hiyo hiyo, kisha atapigiwa Wimbo wa Taifa na dua itasomwa.
Waziri Mkuu, Naibu Spika Alhamisi ya Novemba 16, saa 10 jioni Rais Magufuli anatarajiwa kupeleka kwa Spika jina la Waziri Mkuu ambalo litasomwa mbele ya wabunge wote na kuthibitishwa na wabunge kwa kura.Siku hiyo hiyo, Spika huyo anatarajiwa kuanza kuapisha wabunge na kazi hiyo ataendelea nayo siku ya Jumatano na kumalizia siku ya Alhamisi asubuhi kwa wabunge watakaokuwa hawajala kiapo cha uaminifu.
Baada ya kuthibitishwa kwa Waziri Mkuu, siku hiyo hiyo Naibu Spika atachaguliwa na kula kiapo cha uaminifu na baada ya hapo wabunge watajiweka tayari kwa Hotuba ya Kwanza ya Rais Magufuli itakayotolewa Ijumaa saa kumi jioni na kufuatiwa na kuahirishwa kwa Bunge.
0 comments:
Post a Comment