Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini. Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatano, Tarehe 7 Desemba, 2016. Pamoja na kutambua bei kikomo za bidhaa mbalimbali za petroli nchi nzima, ni muhimu kuzingatia yafuatayo:-
(a) Bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote yaani Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimebadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la tarehe 2 Novemba 2016. Kwa Mwezi Desemba 2016, bei za rejareja kwa Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimeongezeka kama ifuatavyo: TZS 29/lita sawa na asilimia 1.59, TZS 78/lita sawa na asilimia 4.53 na TZS 68/lita sawa na asilimia 4.08 sawia.
Vilevile, kwa kulinganisha na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla kwa mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa nazo zimeongezeka kama ifuatavyo: TZS 29/lita sawa na asilimia 1.68,TZS 78/lita sawa na asilimia 4.84 na TZS 68/lita sawa na asilimia 4.36.
Kuendelea kupanda kwa bei za mafuta kwenye soko la ndani, kwa kiasi kikubwa kumetokana na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia
(b) Bei za jumla na za rejareja kwa mafuta ya Petroli na Dizeli kwa mkoa wa Tanga, nazo zimepanda isipokuwa Mafuta ya Taa ambapo bei imeshuka ikilinganishwa na toleo la bei za mafuta hayo lililopita la tarehe 02 Novemba 2016. Katika toleo hili, bei ya rejareja kwa Petroli na Dizeli zimepanda kama ifuatavyo:
TZS 8/lita sawa na asilimia 0.43 na Dizeli kwa TZS 14/lita sawa na asilimia 0.80, kwa Mafuta ya Taa bei imepungua kwa TZS 3/lita sawa na asilimia 0.16. Aidha, kwa kulinganisha matoleo haya mawili, bei za jumla kwa mafuta ya Petroli na Dizeli mkoa wa Tanga zimepanda kwa TZS 8/lita sawa na asilimia 0.45 na Dizeli TZS 14/lita sawa na asilimia 0.86, na kwa Mafuta ya Taa bei imepungua kwa TZS 3/lita sawa na asilimia 0.17.
Kupungua kwa bei ya Mafuta ya Taa kumesababishwa na kupungua zaidi kwa gharama ya usafirishaji (premium) na kuongezeka kidogo kwa bei ya mafuta haya katika soko la dunia ukilinganisha na mafuta ya Dizeli na Petroli.
(c) Mamlaka inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za mafuta kwa eneo husika, zinapatikana vile vile kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo. Huduma hii ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini.
(d) Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.
(e) Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo ziwe chini ya bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na EWURA na ambayo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 70/2016 la Mwezi Februari 2016.
(f) Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana
bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani.
bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani.
Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.
(g) Wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita. Stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwaa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.
0 comments:
Post a Comment