Ujerumani watashuka dimbani kukwaana na Ukraine kwenye muendelezo wa kinyang’aniro cha kuwania ubingwa wa Euro 2016, katika mchezo wa kundi C utakaopigwa leo kunako dimba la Stade Pierre Mauroy huko Lille majira ya saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Kocha wa Ujerumani Joachim Low amekumbwa na changamoto kufuatia majeraha ya hivi punde ya beki wake wa kutegemewa Mats Hummels.
Ujerumani wanaingia katika michuano hii ikiwa ni mara yao ya 12 tangu kuanzishwa kwake. Mara ya mwisho kushindwa kufuzu ilikuwa ni mwaka 1968 wakati huo ikijulikana kama Ujerumani Magharibi. Wamechukua ubingwa huu mara tatu (1972, 1980 na 1996), na wamepoteza katika fainali tatu (1976, 1992, 2008). Na wamewahi kuishia katika hatua za makundi miaka ya 1984, 2000 na 2004.
Hakika kampeni ya Ujerumani kufuzu kufika hatua hii haikuwa rahisi hata kidogo. Kundi lao lilikuwa likiundwa na mataifa ya Poland, Ireland na Scotland.
Walimaliza kileleni kwa pointi moja juu ya Poland wakishinda mechi saba, sare moja, na vipigo viwili. Kiwango chao katika michezo ya kirafiki ya hivi karibuni kimekuwa si cha kuridhisha, wakipoteza mara mbili mfululizo dhidi ya Ufaransa na Uingereza, lakini wakapata ushindi dhidi ya Italia.
Wakapata kipigo kingine cha mabo 3-1 kutoka kwa Slovakia mwezi Mei na baadaye kupata ushindi dhidi ya Hungary kwenye mchezo wao wa mwisho kwa ajili ya maandalizi ya Euro 2016.
Ukraine wameingia kwenye michuano hii kwa mara ya pili, mara ya kwanza kufanya hivi ilikuwa ni mwaka 2012 wakati walipoandaa michuano hiyo kwa kushirikiana na Polandi.
Kuelekea kufuzu katika michuano hii, Ukraine walimaliza nafasi ya tatu na kucheza playoff dhidi ya Slovenia na kuwatupa nje.
Walimaliza michezo yao hatua ya makundi kwa kushinda mechi 7, droo mbili na kufungwa mara tatu. Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Ukraine kuingia kwa njia ya kufuzu kwenye michuano mikubwa duniani tangu mwaka 2006 walivyofanya hivyo kwenye Kombe la Dunia Ujerumani, ambapo walifanikiwa kufika robo fainali.
Ukraine wanaingia katika mchezo wa leo wakiwa na kiwango kizuri baada ya kushinda michezo yao minne kati ya sita iliyopita. michezo viwili waliyopoteza dhidi ya Uhispania wakati wa kufuzu kuelekea michuano hii inabaki kuwa michezo pekee waliyopoteza kati ya 17 ya mwisho. Hivyo wanaingia katika mchezo huu wa leo wakiwa wanajiamini zaidi.
Dondoo, Historia na takwimu
Ujerumani na Ukraine wamekutana mara tano, Ujerumani wameshinda mara mbili na kutoka sare mara tatu.
Endapo Ujerumani atashinda mchezo huu wa leo, itakuwa ni mara yao ya kwanza kushinda nje ya ardhi ya Ujerumani. Mara zote Ujerumani wamewafunga Ukraine wakiwa katika ardhi yao ya nyumbani. Mechi zote zilizochezwa Ukraine ziliisha kwa sare
Ujerumani na Ukraine walikutana katika mechi za kufuzu kombe la dunia mwaka 1998 nchini Ufaransa. Mchezo huo uliopigwa kwenye mji wa Bremen, Ujerumani walishinda 2-0 (magoli ya Olivier Bierhoff 63’na Mario Basler 71’), mchezo wa marudiano jijini Kiev, walitoka suluhuu
Vile vile walikutana kwenye mechi za mtoano kuelekea Kombe la Dunia mwaka 2002. Mchezo wa kwanza jijini Kiev, walitoka sare ya bao1-1 (magoli yakifungwa na Gennadi Zubov 18’ na Michael Ballack 31’), na mchezo wa marudiano Ujerumani walishinda 4-1 (magoli ya Ballack, 4’ 51’, Oliver Neuville 11’ na Marko Rehmer 15’ huku Ukraine wakipata goli la kupitia kwa Andri Shevchenko 90
Mechi ya ya mwisho kukutana ilikuwa ni ya kirafiki iliyochezwa Kiev Novemba 11 mwaka 2011 na kumalizika kwa sare ya 3-3.
Wachezaji wawili wanaocheza Besiktas Mario Gomez (Ujerumani) na Denis Boyko (Ukraine) wanakutana. Endapo atafunga, Gomez atakuwa mchezaji wa tatu katika historia ya michuano ya Euro kufunga dhidi ya kipa wa klabu yake. Wengine waliowahi kufanya hivyo ni pamoja na Paul Gascoigne dhidi ya mchezaji mwenza wa Rangers Andy Goram mwaka 1996, Samir Nasri dhidi ya mchezaji mwenza Joe Hart mwaka 2012.
Ujerumani: Kikosi kinatachotarajiwa (4-2-3-1)
Neuer, Hector, Mustafi, Boateng, Can, Khedira, Kroos, Gotze, Ozil, Muller, Gomez.
Ukraine: Kikosi kinatachotarajiwa (4-2-3-1)
Pyatov, Shevchuk, Khacheridi, Rakitskiy, Fedetskiy, Garmash, Stepanenko, Konoplyanka, Sydorchuk, Yarmolenko, Zozulya.
Ungana na mimi kupitia Facebook , Twitter na
Instagram Pia subscribe Youtube ili uwe wa kwanza kupata
habari mpya.
0 comments:
Post a Comment