Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema Chadema inawasumbua kutokana na madai yao ya mara kwa mara, lakini chama hicho kikuu cha upinzani hakijakoma; kimeitaka Tume kujibu mambo matano kuhusu Uchaguzi Mkuu.
Chadema, ambayo inashiriki Uchaguzi Mkuu ikiwa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), pia kimesisitiza kuwa wanachama na wafuasi wake wataendelea kukaa mita 100 kutoka vituo vya kupigia kura kama walivyoagizwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe
Chadema imekuwa ikitoa matamko mbalimbali yanayoonyesha wasiwasi kuwa uchaguzi hautakuwa huru na wa haki na katikati ya wiki, walitaka NEC iwakubalie waende na wataalamu wao wa Tehama pamoja na waangalizi wa kimataifa ili kukagua mfumo ambao Tume itautumia kupokea matokeo kutoka vituoni.
Ombi hilo lilimfanya mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva kusema Chadema inawasumbua, akieleza kuwa kila wanapofanya jambo, chama hicho hufanya kitu kingine.
Jana, Chadema iliibuka na tamko jingine ikiitaka Tume kujibu mambo matano kuhusu uchaguzi ambao utafanyika Oktoba 25.
“Tunataka kila jambo liwekwe wazi,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati akiongea na waandishi wa habari jana.
Mnyika alisema Chadema inaitaka Tume hiyo kutaja tarehe watakayovipatia vyama vya siasa nakala pepe ya Daftari la Kudumu la Wapigakura, na tarehe ambayo vyama vitakwenda ofisi za NEC na wataalamu wao wa Tehama kukagua programu itakayotumiwa kuhesabu kura.
Pia alisema wanataka maelezo ya sababu za tume hiyo kupinga wananchi kukaa mita 100 kutoka vituo vya kupigia kura, kutaka maelezo kama vyombo vya habari na wadau wengine wataruhusiwa kujumlisha matokeo ya uchaguzi huo na sababu za kubagua wanahabari kufika katika vituo vya kupigia kura badala yake kutaka wale wenye vitambulisho vya serikali pekee.
Wakati chama hicho kikiibuka na masuala hayo, Jaji Lubuva alisema watakutana na vyama vyote vya siasa kati ya Oktoba 8 na 10 kufafanua masuala mbalimbali, huku akisisitiza kuwa tatizo la Chadema ni kutaka kuingia jikoni na kujua kila jambo linalofanywa na tume.
Katika ufafanuzi wake wa jana, Mnyika alisema: “Kwanza, tunataka tupewe nakala za daftari la wapigakura za awali na za sasa ili tuhakiki kama hakuna majina feki. Tunataka daftari hili liwe wazi pia ili wananchi wahakiki majina yao maana yale yanayobandikwa katika vituo vya kupigia kura ambayo NEC wamesema yatabandikwa siku ya nane kabla ya uchaguzi ni orodha tu.”
Alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, vyama vya siasa vilipewa nakala hizo mapema na kuzihakiki, akifafanua kuwa faida ya daftari hilo kutolewa mapema ni kuwapa fursa wananchi ambao majina yao hayataonekana kufuatilia mapema ili kutopoteza haki yao ya kupigakura.
“Pili, tunataka NEC iseme siku ambayo wataalam wetu watakwenda kukagua programu itakayotumiwa na tume kuhesabu kura. Tunataka mifumo yote miwili waliyoisema tuihakiki kama ipo sawa kuepusha uchakachuaji wa matokeo na tunafanya hivi kwa sababu mifumo iliyotumika 2010 ilikuwa mibovu,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema jambo la tatu ni kupingana na kauli za kuwazuia wananchi kukaa mita 100 kutoka vituo vya kupigia kura akisema suala hilo ni lazima liruhusiwe ili kuwapa fursa wananchi kulinda kura zao zisiibiwe.
Alisema jambo jingine ni NEC kueleza kama vyombo vya habari, asasi za kiraia na waangalizi wa uchaguzi wataruhusiwa kujumlisha matokeo.
“Hili jambo ni muhimu maana matokeo ya urais hayahojiwi mahakamani, hivyo ni lazima tudhibiti ujanja ujanja mapema,” alisema.
Akijibu madai yaliyotolewa na Chadema, Jaji Lubuva alisema: “Kama wana malalamiko wayalete ofisini kwetu. Siwezi kujibu malalamiko yanayowasilishwa katika mikutano ya waandishi wa habari. Kifupi ni kwamba tutakutana na vyama vyote vya siasa kuvieleza tulipofikia. Hawa Chadema wanatusumbua sana hawa.”
Kauli ya Kova
Wakati Chadema ikisisitiza msimamo wao, kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jeshi hilo limejipanga ipasavyo kuelekea siku ya kupiga kura, akisema watakaobainika kukiuka sheria na taratibu za uchaguzi watachukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.
“Tunaomba kila mmoja kufuata utaratibu utakaowekwa. Atakayeuvuruga hatutasita kumchukulia hatua. Tunataka uchaguzi ufanyike kwa amani na kila mmoja mwenye haki ya kupiga kura, apige kwa amani,” alisema.
Kuhusu taarifa za kiitelijensia za kuwepo na watu kufanya vurugu, Kamishna Kova alisema hawezi kurudia maneno yaliyosemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, aliyesema watakaovunja sheria watakumbana na mkono wa sheria.
Sadiki alonga
Sadiki alisema kuwa kuna vikundi vimejipanga kufanya vurugu kwenye uchaguzi na akavitaka kuacha mara moja kwa kuwa Serikali ya Mkoa imejipanga kukabiliana navyo.
Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa hakuwa tayari kuvitaja vikundi hivyo wala kufafanua vinaratibiwa na nani.
Akifungua semina ya mafunzo ya siku mbili ya wasimamizi 60 wa Uchaguzi Mkuu kutoka wilaya tatu za Kinondoni, Temeke na Ilala, Sadiki alisema vikundi hivyo vinatoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.“Tumejipanga kisawasawa kukabiliana na aina yoyote ya vurugu siku hiyo,” alisema Sadiki.
“Lengo lao kubwa ni kuwatisha watu watakaopiga kura hususani kinamama na wazee. Nawaomba waache mara moja kwani wakibainika watapambana na mkono wa dola.
“Tunayatambua maeneo ambayo watapelekwa na tutahakikisha ulinzi unaimarishwa kwani tumejipanga ipasavyo.”
Alisema mbali na hivyo, kundi jingine limejipanga kukaa mita 100 kutoka katika kituo cha kupigia kura na kwamba wamepata taarifa kuwa watajipakaa rangi zenye mfano wa damu na kuwatisha wananchi kwa kuwaambia kuna machafuko kutokana na mwonekano wao.
“Nawaomba wakishapiga kura, wananchi waondoke mapema vituoni. Ingawa sheria inaruhusu kukaa mita 100, tunataka kupambana na mbinu hizi zilizopangwa,” alisema Sadik.
Pia aliwataka wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia uwazi na kuhakikisha vituo vinafunguliwa mapema ili kuondoa wasiwasi kwa wapigakura
0 comments:
Post a Comment