Ripoti ya utafiti imeonyesha kuwa wanawake wengi hufanyiwa vitendo vya unyanyasaji ikiwamo kutolewa lugha chafu wawapo sokoni.
Utafiti huo uliofanywa na Shirika lisilo la kiserikali la Equality for Growth (EfG) la jijini Mwanza mwaka 2014 hadi 2015, umebaini kuwa licha ya kuwa na idadi kubwa la wanawake katika masoko kulinganisha na wanaume, ni asilimia 10 pekee ya wanawake ndiyo hupewa fursa za uongozi katika masoko.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita, Mratibu wa Shirika la EfG Mkoa wa Mwanza, Ikupa Mwakisu alisema utafiti huo ulifanyika katika Soko Kuu la Jiji la Mwanza na lile la Makuyuni.
“Ukatili unaoongoza kwa wanawake sokoni ni maneno na lugha chafu kutoka kwa wanaume,” alisema Mwakisu.
Mfanyabiashara, Pili Mussa anashauri elimu itolewe kwa wanawake na wanaume wafanyabiashara katika masoko yote kukabiliana na ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake.
“Pamoja na kukosa elimu na mwamko wa kuwania fursa za uongozi, mila na desturi zinazomchukulia mwanamke kama kiumbe duni kulinganisha na mwanaume pia inachochea sisi (wanawake), kunyimwa fursa za uongozi katika kamati za soko,” alisema Mussa
0 comments:
Post a Comment