KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, atatua ofisini kwa kiongozi mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, ili kumueleza mkakati wake wa kutua ofisini kwake, Buguruni jijini Dar es Salaam
Maalim anakwenda kwa IGP Mangu kumueleza adhima yake ya kufika ofisi kuu ya chama chake kesho Ijumaa, majira ya saa mbili asubuhi.
Hatua ya Maalim kutinga ofisini kwa IGP imetokana na kitendo cha jeshi la polisi kumsindikiza Prof. Lipumba kurejea ofisini; kusaidia uharibifu wa mali na kushambulia wanachama na wafuasi wa chama hicho.
Azma yake ya kwenda ofisini kwake kesho, inatokana na ofisi hiyo kuvamiwa na aliyepata kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba na genge la wafuasi wake.
Prof. Lipumba aliyejiuzulu uenyekiti wa CUF, 6 Agosti mwaka jana na miezi 11 baadaye akatangaza kurejea katika nafasi yake, amefukuzwa rasmi uanachama wa chama hicho Jumanne iliyopita na Baraza Kuu la uongozi la Taifa (BKT), lililokutana Visiwani.
Hata hivyo, Prof. Lipumba, ameendelea kung’ang’ania kuwa bado mwenyekiti halali wa chama hicho na msimamo wake huo, unadaiwa kuungwa mkono na msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa watu waliokaribu na Maalim Seif zinasema, kiongozi huyo amekwenda kwa IGP Mangu kumtaarifu kuwa yeye na wabunge wa chama hicho, wamepanga kufika Buguruni kwa pamoja.
Anasema, “Maalim Seif anakwenda kumweleza IGP Mangu kwamba, tayari kumekuwepo na viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na watu wa Prof. Lipumba na kwamba chochote kitakachotokea, yeye na jeshi lake, wanapaswa kubeba msalaba.”
Prof. Lipumba alijiuzulu uenyekiti karibu na uchaguzi mkuu mwaka jana, akakimbilia nje ya nchi huku akidai hakufurahishwa na Edward Lowassa kuwa mgombea urais chini ya mwavuli wa vyama vinne ikiwamo CUF.
Ukawa unaundwa na vyama vinne; Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na National League for Democrats (NLD).
0 comments:
Post a Comment