Mechi hiyo iliyokuwa na ushindani wa hali ya juu, imeshuhudia Simba wakianza kwa kasi na kuonesha ari ya kupata mabao ya mapema, lakini ngome ya JKT Ruvu ilionesha uimara wa aina yake kwa kuwazuia washambuliaji machachari wa Simba, Shiza Kichuya, Laudit Mavugo na Fredrick Blagnon.
JKT Ruvu nao walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza na kusababisha hatari kadhaa langoni mwa Simba, lakini hadi dakika 45 zinakatika, hakuna timu iliyoweza kupata bao.
Kipindi cha pili Simba ilimtoa Blagnon na kuingia Ibrahim Ajibu na Mwinyi Kazimoto aliyechukua nafasi ya Jamal Mnyate, mabadiliko ambayo yaliongeza kasi zaidi kwa Simba ambapo katika dakika za majeruhi, lango la JKT Ruvu lilikuwa kwenye wakati mgumu kwa kukabiiwa na michomo lukuki, lakini safu ya ulinzi ya maafande hao ilisimama imara na kufanya matokeo hadi mwisho wa mchezo kuwa 0-0.
Katika mchezo uliopigwa Chamazi Dar eSalaam, Azam imetumia vyema maji ya wanalizombe Majimaji ya Songea kutengenezea 'Ice Cream' kwa kuichapa mabao 3-0, na kunyakua point 3 muhimu.
Magoli ya Azam yamefungwa na nahodha wake John Bocco aliyefunga mabao mawili katika dakika za 2 na ya 83, huku kiungo Mudathir Yahya akiifungia bao la pili katika dakika ya 16.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Mwaadui FC imepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC katika mchezo ulipigwa dimba la CCM Kirumba Mwanza, kwa bao lililofungwa na Abdallah Seseme.
Mkoani Morogoro Mtibwa Sugar imejifuta machozi baada ya leo kupata ushindi wa maba 2-1 dhidi ya Ndanda FC. Ikumbukwe katika mchezo wa Kwanza Mtibwa walifungwa na Ruvu Shootinga bao 1-0 katika uwanja huohuo wa Manungu.
Kagera Sugar imetoka suluhu la bila kufungana, huku Ruvu Shooting na Tanzania Prisons wakitoka sare ya bao 1-1.
Ligi hiyo itaendelea kesho katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam kwa mchezo mmoja utakaozikutanisha Yanga na African Lyon.
Ungana na mimi kupitia Facebook , Twitter na
Instagram Pia subscribe Youtube ili uwe wa kwanza kupata
habari mpya.
0 comments:
Post a Comment