www.kenethngamoga.blogspot.com

PRO LIPUMBA ARUDI CUF,UONGOZI WATOA TAMKO

PROFESA Ibrahim Lipumba, aliyetangazwa kusimamishwa uanachama na Chama cha Wananchi (CUF), ametangazwa kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho, anaandika Faki Sosi via MwanaHALISI Online.
Taarifa ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini iliyotolewa jana na kusambazwa leo imeeleza kuwa, Prof. Lipumba bado ni mwenyekiti wa chama hicho kwa mujibu wa taratibu.

“Baada ya upembuzi wangu ni kuwa, Lipumba bado mwenyekiti halali wa CUF na waliofukuzwa, kusimamishwa ni wanachama halali.

“Viongozi ambao uamuzi wao uliathirika na maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa bado ni viongozi halali wa CUF,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa Jaji Francies Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Prof. Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho Agosti mwaka jana kwa madai ya kutoridhishwa na ujio wa Edward Lowassa ambaye baadaye aliteuliwa kuwa mgombea urais wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Katika Ofisi Kuu ya chama hicho iliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam, wafuasi wa Prof. Lipumba mchana huu wamefurika wakimsubiri na kwamba, yupo njiani kwenda ‘ofisini kwake.’

Agosti mwaka huu CUF ilimsimamishwa uanachama Prof. Lipumba kwa tuhuma za kuwa kinara wa vurugu zilizosababisha mkutano mkuu maalum wa chama hicho kuvunjika.

Mkutano huo ulifanyika katika Hotel ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam, Prof. Lipumbana wafuasi wake waliuvamia na kusababisha kuvunjika.

Pamoja naye katika adhabu hiyo ni viongozi waandamizi wengine 10 akiwemo Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kaliua; Maftaha Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini na Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma.

Uamuzi huo ulitangazwa rasmi Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, wakati akitoa taarifa ya Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa (BKUT), kilichofanyika mjini Zanzibar mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi wengine waliochukuliwa hatua hiyo hadi watakapojieleza mbele ya Baraza Kuu hilo, ni Ashura Mustafa, Omar Mhina Masoud, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.

Wakati Ashura ni mjumbe wa Baraza Kuu na mwanamama aliyewahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa chama, Mnyaa na Kombo ni viongozi wazoefu waliokuwa wabunge kipindi cha 2010/2015; Mnyaa akiwakilisha Jimbo la Mkanyageni na Kombo Jimbo la Chake Chake, kisiwani Pemba.


Kufuli zavunjwa, risasi zarindima CUF


RISASI za moto zimerindima katika Ofisi Kuu ya Chama cha Wananchi (CUF) Buguruni, jijini Dar es Salaam leo mchana, wakati Prof. Ibrahim Lipumba alipowasili ili kuanza rasmi kazi baada ya kupokea barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa inayomtambua kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho, anaandika Charles William via MwanaHALISI Online.

Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, katika barua yake iliyoandikwa 23 Septemba mwaka huu, ameeleza kumtambua Prof. Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF na kwamba, viongozi wa CUF walioteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho 28 Agosti mwaka huu si halali.

Katika mapokezi yake, wafuasi wa Prof. Lipumba walijipanga kuanzia Barabara ya Buguruni (Rozana) inayoingia Ofisi Kuu za chama hicho na kuimba huku wakipuliza matarumbeta. Ilikuwa saa 7:00 mchana ambapo dakika ishirini na mbili baadaye kiongozi huyo alifika katika barabara hiyo akiwa katika gari aina ya Rav 4 yenye Na. T 639 AZK.

Baada ya wafuasi wake kumlaki, Prof. Lipumba alishuka na kuanza kutembea kwa mguu sambamba na wafuasi wake hadi ofisi za chama hicho zilizopo umbali wa takribani mita 300 kutoka barabarani hapo.

Wafausi hao walimsindikiza wakiimba nyimbo mbalimbali za chama hicho ikiwemo nyimbo yao maarufu, “Ooooh chamaaa… chama gani? Chama cha Wananchi CUF, Oooh chamaaa… chama gani? Chama cha Wananchi CUF.”

Walikutana na kundi lingine kubwa katika ofisi hiyo, hata hivyo geti la lango kuu lilikuwa limefungwa hivyo Prof. Lipumba alishindwa kuingia.

Baada ya kupita dakika tano tangu kuwasili Prof. Lipumba katika eneo hilo, zaidi ya wafuasi wake 20 waliparamia ukuta na kuingia ndani ya ofisi hiyo kisha kuwakabili walinzi waliokuwa wamefunga geti hilo na kisha walilivunja.

Baada ya walinzi kuzidiwa nguvu, walikimbia kwa kuruka ukuta na kudondokea nyumba za jirani na kutokomea, mmoja wa walinzi hao alinyang’anywa bunduki na wafuasi hao. Baada ya kuvunjwa kufuli la geti la lango kuu, Prof. Lipumba na kundi kubwa la wafuasi wake waliingia ndani huku wakishangilia.

Wakati hayo yakitendeka, polisi walikuwa nje ya ukuta wa ofisi hiyo ndani ya gari lao lenye namba PT 3699 wakiwa na silaha za moto. walikuwa watulivu ndani ya gari hiyo bila kuchukua hatua zozote. Baada ya muda mchache gari nyingine ya polisi yenye Na. T 709 ASF iliwasili ili kuongeza ulinzi.

Mara baada ya Prof. Lipumba kuingia ndani, polisi nao waliingia ndani kwa lengo la kuichukua bunduki iliyokuwa mikononi mwa wafuasi wa Lipumba. Wakati huo risasi za moto zilipigwa hewani kutokana na sintofahamu iliyokuwepo eneo hilo.

Hata hivyo, Prof. Lipumba hakuweza kuingia ndani ya ofisi kutokana na mlango wa kuingia ndani kufungwa, wafuasi waliamua kuvunja kufuli kwa nguvu chini ya usimamizi wa polisi na hatimaye aliingia ndani.

Mkuu wa askari hao aliokuwa amevaa kiraia sambamba na mwingine mwenye jina MADALI S.B walishuhudia tukio hilo, katika hali ya kushangaza askari aliyevalia kirai aliyeonekana kuwa kiongozi w polisi hao, alitishia kuvunja kamera za wandishi wa habari watakaompiga picha.

Prof. Lipumba aliingia ndani ya ofisi yake na kuzungumza na waandishi wa habari akisema, “nimerejea kazini na nawasihi wana CUF wawe wamoja, wasahau yaliyopita tukijenge chama chetu.”

Lipumba aliongea kwa muda mfupi na waaandishi hao kabla ya kutoka nje kuzungumza na wafuasi wake, ambapo amewatahadharisha viongozi wa muda waliowekwa na kikao cha baraza kuu la chama hicho 28 Agosti mwaka huu kukaa mbali na shughuli za chama hicho.

Lipumba amesema, “Nataka kujenga chama kitakachoenea kila mahali si chama cha upande mmoja tu, sina tatizo na viongozi wa CUF waliochaguliwa na wanachama katika uchaguzi mkuu.”

Pof. Lipumba aliwaaga wanachama wake na kuwasihi kumpa ushirikiano ili aweze kukijenga chama hicho. Hata hivyo katika hali ya kushangaza gari yake aliyokuja nayo Na. T 639 AZK iligoma kuwaka nay eye kushindwa kuondoka katika eneo hilo.

Tukio hilo lilitokea saa nane na dakika arobaini mchana (8:40) na ilimlazimu Prof. Lipumba kukaa kwa zaidi ya dakika 10 gari hilo liweze kuwashwa, lakini halikuweza kuwaka na hivyo kulazimika kupanda gari linguine Na. T 581 CJU ambalo lilikuwepo katika eneo hilo.

Haikujulikana mara moja gari hiyo ni mali ya nani, Prof. Lipumba aliondoka katika eneo hilo huku ndani ya gari hiyo akiwa ameambatana na watu wengine wanne na magari matatu yenye askari polisi yakimsindikiza nyumba.

Magari yaliyomsindikiza nyuma wakati Prof. Lipumba akiondoka katika eneo la ofisi kuu za CUF, Buguruni majira ya saa nane na dakika hamsini (8:50) ni pamoja na lile lenye namba za usajili PT 3891, PT 3699 na T 709 ASF.

Hivi punde tutakuletea kwa kirefu kile alichoongea Prof. Lipumba mbele ya wafuasi wake.

------------

wavuti.com imepata taarifa kutoka WhatsApp kama inayoendelea hapa chini...




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tarehe: 24 Septemba, 2016

The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kimepokea kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kile kinachoitwa “Msimamo na Ushauri wa Vyama vya Siasa kuhusu Mgogoro wa Uongozi wa Kitaifa wa Chama cha Civic United Front (CUF)” ambao uliwasilishwa Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, jana usiku.

Baada ya kupokea Ushauri huo, The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kinapenda kueleza yafuatayo:

1. Sheria ya Vyama vya Siasa (Political Parties Act, No. 5 of 1992) haimpi mamlaka wala uwezo wowote Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi ya vikao vya Chama.

2. Msimamo huo wa kisheria wa nchi hii umetiliwa nguvu na kuthibitishwa na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia UAMUZI wa tarehe 9/5/2005 wa Jaji T.B. Mihayo katika kesi ya Emmanuel Nyenyemela na Magnus Msambila v/s Registrar of Political Parties & Others (Civil Case No. 6 of 2003) ambapo Jaji Mihayo aliamua kwamba:

“… I do not see anywhere in the Political Parties Act where the Registrar has power to bless or condemn meetings of political parties or decisions that they make.”

Tafsiri ya uamuzi huo ni kwamba, “… Sioni popote katika Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo Msajili ana madaraka ya kubariki au kupinga vikao vya vyama vya siasa na maamuzi ambayo vikao hivyo vinafanya.”

3. Kwa msingi huo, CUF hatukuomba ushauri kwa Msajili na hivyo tunamwambia ushauri wake abaki nao mwenyewe.

4. Kwa msingi huo huo, tunawataka wanachama wa CUF na wananchi wote kutambua kwamba Msajili hana uwezo kisheria wa kusikiliza mashauri yanayohusiana na malalamiko dhidi ya maamuzi ya vikao vya vyama vya siasa na na kuyatolea uamuzi. Uwezo huo ni wa Mahakama. Hivyo tunawataka wanachama wa CUF na wananchi wote kupuuza ushauri huo wa Msajili na wamwachie mwenyewe ndoto zake na propaganda za kitoto.

5. Ni fedheha na aibu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa mwenye hadhi ya Ujaji kukubali kutumiwa kiasi hicho na kushindwa hata kufanya rejea kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu tulioutaja hapo juu ambao umeweka bayana kwamba hana madaraka na uwezo aliojifanya anao. Itakumbukwa kwamba Wabunge wa CUF walifanya mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma tarehe 15 Septemba, 2016 na kumtahadharisha Msajili asikubali kutumiwa kufanya alichokuwa anatakiwa kukifanya. Ni bahati mbaya sana kwamba amefanya kile kile ambacho Wabunge wa CUF walieleza kwamba walikuwa na taarifa kuwa ameagizwa kukifanya.

6. Tunajua kwamba baada ya hatua hiyo ya Msajili kufanya kazi asiyo na uwezo wala mamalaka nayo na katika kutimiza malengo ya wanaotuma, mchana wa leo Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake cha wahuni kimevamia Ofisi Kuu ya CUF, Buguruni, Dar es Salaam na kupiga watu na kufanya uharibifu wa mali. Tunamwambia Msajili wa Vyama vya Siasa atabeba dhamana kwa yote yaliyofanywa na yatakayofanywa na kikundi hicho ikiwemo watu watakaoumizwa na uharibifu wa mali utakaofanywa kutokana na tamko lake hilo ambalo halina msingi wa kisheria.

7. Tunatambua yote haya yanafanywa kwa sababu watawala wameingiwa kiwewe kutokana na hatua kubwa ambazo zimefikiwa na CUF katika kupigania haki yake ya ushindi ulioporwa katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015. CCM haijakaa sawa tokea iliposhindwa vibaya na CUF katika uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani mwaka 2015 na sasa imepata mfadhaiko kutokana na jinsi jumuiya ya kimataifa ilivyosimama kidete kutetea maamuzi hayo ya

kidemokrasia na haki za binadamu za Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla. Ni vyema watawala na kibaraka wao Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake pamoja Msajili anayewatumikia wakatambua kwamba CUF haiyumbishwi na michezo yao ya kitoto na itaendelea kusimamia malengo yake ya kupigania haki za kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar na Tanzania kikamilifu.

8. Chama kinasisitiza tena kwamba maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe 21 Agosti, 2016 na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la tarehe 28 Agosti, 2016 ni halali na yako pale pale na kwamba Prof. Ibrahim Lipumba si Mwenyekiti wa CUF na wanachama waliosimamishwa au kufukuzwa wataendelea kubakia wamesimamishwa au kufukuzwa isipokuwa tu iwapo vikao vya Chama vitakapofanya maamuzi mengine.

9. Chama kinawataka viongozi wake wote na wanachama wake katika ngazi zote kuanzia Taifa hadi Tawi kuendelea na kazi zao za ujenzi wa Chama kama kawaida na kuendelea kufuatilia harakati za Chama chao kupigania ushindi wetu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.

HAKI SAWA KWA WOTE

NASSOR AHMED MAZRUI

NAIBU KATIBU MKUU - CUF

Ungana na mimi kupitia Facebook , Twitter na Instagram Pia subscribe Youtube ili uwe wa kwanza kupata habari mpya.
Share on Google Plus

Keneth Ngamoga

Keneth Ngamoga ni mtangazaji wa radio Pambazuko iliyopo Ifakara.Huwa akisikika katika vipindi tofauti vya burudani.Kwa msaada na ushauri Wasiliana na Keneth Ngamoga Kupitia namba
+255655632798
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment