www.kenethngamoga.blogspot.com

Simanzi Zatawala >>mwili wa Kombani warejeshwa nyumbani

SIMANZI, majonzi na vilio vilitawala jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, wakati ndege ya Shirika la Ndege la Emirates, iliyobeba mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani (pichani), ilipokuwa ikitua katika uwanja huo.
Kabla ya kutua kwa ndege hiyo, mamia ya waombolezaji waliofika kiwanjani hapo walikuwa wakizungumza hili na lile, lakini ndege hiyo ilipoanza kutua saa tisa na dakika 32 alasiri, kulitokea kimya huku kila mmoja akitafakari na wengine wakifuta machozi, wakati wakisubiri mwili wa waziri huyo aliyefariki akiwa nchini India kwa matibabu ya saratani.

Wakizungumza kwa majonzi kiwanjani hapo baada ya kupokea mwili huo, baadhi ya mawaziri walisema kifo hicho kimekuwa cha ghafla mno kwani wamempoteza kiongozi mahiri na mgombea ubunge aliyependwa na wananchi wa Jimbo la Ulanga Mashariki.
*Saada
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema msiba huo umemgusa binafsi na ni pigo kwa Serikali pia, kwani Kombani alikuwa kiongozi mahiri na mchapakazi. “Ni msiba ulionigusa, kwa kweli Kombani alikuwa mchapakazi, mara nyingi alinishirikisha na kunishauri kiutendaji serikalini, ni pigo kwa Serikali na jamii,” alisema Mkuya.
*Kinana
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana alisema msiba huo ni mkubwa na ni pigo kwa chama hicho na wananchi wa Morogoro, kwani pamoja na kwamba kifo ni kifo, ila hicho cha Kombani kimetokea ghafla mno.
“Ni msiba mkubwa, kwetu na kwa wananchi wa Morogoro lakini kubwa zaidi kwa familia yake, kifo ni kifo ila hiki cha Kombani kimekuja ghafla, tulikuwa na imani atashinda kwa kishindo jimboni kwenye uchaguzi ujao,” alisema Kinana.
*Sefue
Akizungumzia msiba huo Katibu Mkuu kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema kifo cha Kombani ni pigo kwa Serikali na jamii kutokana na uhodari wake wa kuchapa kazi akiwa mtumishi wa umma.
“Ni pigo kwa Wizara na serikali na pia kwa jamii, tumempoteza mbunge mahiri aliyetetea vyema maslahi ya wananchi wake jimboni na serikali yake,” alisema Sefue.
*Kampeni zasitishwa
Wakati huo huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imesitisha uchaguzi kwenye jimbo la Ulanga Mashariki, ambalo Kombani alikuwa mmoja wa wagombea nafasi ya ubunge na kufanya hadi sasa majimbo yaliyosimamishwa kampeni kwa ngazi hiyo, kuwa mawili, likiwemo Jimbo la Lushoto.
Kusitishwa huko kumethibitishwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima, ambaye alikuwa miongoni mwa waombolezaji waliofika kiwanjani hapo kupokea mwili wa Kombani.
Alisema kifo cha Kombani ni pigo kwa Taifa lakini pia kwa NEC, kwani wamempoteza mmoja wa wagombea ambao tume hiyo iliwapitisha na walishitushwa na taarifa za kifo hicho. “Tulishitushwa sana na taarifa za kifo cha mgombea huyo, kwa kweli jamii na Taifa limeondokewa na mtu muhimu,” alisema Kailima.
Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Sura ya 343, ndani ya siku 30 tangu msiba kutokea, chama kilichopoteza mgombea kinatakiwa kiteue mgombea mwingine na NEC itapaswa kufuata taratibu husika ili kupitishwa kuwa mgombea wa nafasi hiyo.
Alisema kuanzia sasa wameahirisha uchaguzi na kampeni jimbo hilo hadi watakapotangaza upya tarehe ya uchaguzi na kusisitiza kuwa katika Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu jimbo hilo na lile la Lushoto hayatakuwemo kwenye uchaguzi.
*Viongozi wengine
Viongozi wengine waliofika kupokea mwili wa Kombani kiwanjani hapo ni pamoja na mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma, baadhi ya mawaziri wakiwemo Waziri wa Elimu, Dk Shukuru Kawambwa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia.
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angela Kairuki.
Pia alikuwepo mgombea mwenza wa CCM-Zanzibar, Samia Suluhu, Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadik, viongozi wengine mbalimbali, pamoja na jamaa wa marehemu.
Aidha, taarifa kutoka Ofisi ya Bunge iliyopatikana kiwanjani hapo, ilieleza kuwa mipango ya mazishi inaendelea kufanywa na tarehe rasmi ya maziko yatakayofanyika Morogoro, itatangazwa hapo baadaye, ila kwa jana mwili ulipelekwa nyumbani na baadae kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi

Jiunge na mimi kwenye FACEBOOK , TWITTER & INSTAGRAM Usikose kusubscribe kwenye you tube kwa kubonyeza>>>VIDEO

Ungana na mimi kupitia Facebook , Twitter na Instagram Pia subscribe Youtube ili uwe wa kwanza kupata habari mpya.
Share on Google Plus

Keneth Ngamoga

Keneth Ngamoga ni mtangazaji wa radio Pambazuko iliyopo Ifakara.Huwa akisikika katika vipindi tofauti vya burudani.Kwa msaada na ushauri Wasiliana na Keneth Ngamoga Kupitia namba
+255655632798
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment